Kagera Sugar Yashindwana na Kaseja Yamruhusu Kwenda Popote
NI kama uongozi wa Kagera Sugar umeamua kumruhusu mlinda mlango wao mahiri, Juma Kaseja, kujiunga na timu yoyote ambako ataona yeye kunamfaa baada ya kushindwana na uongozi wa timu hiyo.
Kaseja ambaye alishawahi kuzitumikia klabu za Simba na Yanga kabla ya kujiunga na Mbeya City na kisha kujiunga na Kagera Sugar ameshaelezwa kuwa anaweza kuondoka hapo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein, alisema kuwa walikaa kikao jana kujadili juu ya kuongeza wachezaji wapya katika timu yao baada ya kocha wao kuwasilisha ripoti yake juzi.
“Mwalimu alitupatia ripoti Jumapili baada ya kumaliza sikukuu ya Eid na Jumatatu tulikaa kikao na viongozi wengine na yeye kocha (Mecky Mexime), nadhani hatutasajili wachezaji wengi ila tutaangalia wachezaji ambao wataondoka, lazima tuangalie wachezaji mbadala.
“Juma Kaseja tupo naye kwenye mazungumzo, lakini kama atapata timu ya kwenda, tunamruhusu kwenda.
“Sisi tunaamini kuna wachezaji wengi wenye kipaji kama Kaseja, hatuwezi kumlazimisha mchezaji kama anataka kuondoka.
“Sisi siyo kama timu nyingine kwamba tunapatana na mchezaji tutampa kiasi hiki, hatuwezi kuvuka hapo hata aje nani na huo ndiyo utaratibu wetu, sasa kama ameona sehemu kuna maslahi sisi tunamruhusu kwenda,” alisema.
Comments
Post a Comment