Sababu ya kuachiwa Babu Tale ni kuwa amri ya kumkamata yeye na ndugu yake Idd Shaban Taletale ilitolewa kimakosa
Sababu za kuachiwa Hamis Shaban Taletale maarufu kama Babu Tale mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection, aliyekuwa akisota mahabusu, akisubiri amri ya kupelekwa kifungoni gerezani, zimebainika.
Babu Tale ambaye pia ni meneja wa mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul, ‘Diamond Platnumz’, aliachiwa kwa muda na Jaji Edson Mkasimongwa, kwa kile kilichoelezwa kuwa amri ya kumkamata yeye na ndugu yake Idd Shaban Taletale ilitolewa kimakosa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka mahakamani hapo, makosa yaliyobainika katika amri hiyo ni kwamba aliyeitoa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam, Wilbard Mashauri hakuwa na mamlaka ya kutoa amri hiyo na kwamba ilikuwa haieleweki.
Hivyo Jaji Mkasimongwa alimwachia jana kwa muda lakini akamtaka afike mahakamani saa 6:00 mchana, leo Mei 25, 2018.
Babu Tale alitiwa mbaroni Jumanne Mei 22, 2010, kwa amri ya mahakama hiyo iliyotolewa na Naibu Msajili Mashauri Februari 16 na hati ya kuwakamata iliyotolewa April 4, 2018, ili kuwapeleka kifungoni katika gereza la Ukonga, kutokana na kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama hiyo.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016, iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini la Kiislam Sheikh Hashim Mbonde, kutokana na makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.
Wakati anaachiwa jana saa 11:40, mdai wake Sheikh Mbonde hakuwepo mahakamani hapo wala wakili wake Mwesigwa Muhingo.
Hivyo Jaji Mkasimongwa alimwelekeza Babu Tale amtaarifu wakili wa mdai wake afike mahakamani pamoja na mdai kwa ajili ya kusikilizwa pande zote, kabla ya uamuzi mwingine.
Alipoulizwa baadaye na Mwananchi sababu ya kutokuwepo mahakamani hapo wakati mdaiwa wake alipopelekwa, Sheikh Mbonde alisema yeye na wakili wake hawakuwa na wito wa kufika mahakamani hapo wala kuwa na taarifa kama mdaiwa wake alipelekwa tena mahakamani.
Sheikh Mbonde alilieleza Mwananchi kuwa jana yake alipigiwa simu na RCO akamtaka afike ofisini kwake na wakakubaliana kuwa angefika kesho yake.
Aliongeza kuwa jana asubuhi alipowasiliana na RCO, alimweleza kuwa walikuwa na ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya ufunguzi wa vituo mbalimbali vya Polisi na kwamba baada ya shughuli hiyo ndipo angempa maelekezo mengine, lakini mpaka wakati huo alikuwa hajapata maelekezo yoyote.
Jana Babu Tale alifikishwa mahakamani hapo muda wa saa Nne asubuhi, ikiwa ni mara ya tatu kufikishwa mahakamani kwa ajili ya mahakama kutoa amri ya kumpeleka kifungoni, kwa mujibu wa amri na hati ya kuwakamata yeye na ndugu yake.
Jana alipofikishwa alisubiri mahabusu hadi saa 9:40, wakati Naibu Msajili Ruth Massam alipowaita mawakili wa pande zote na askari polisi waliompeleka Babu Tale. Kwa kuwa mdai na wakili wake hawakuwepo basi ni wakili wa Babu Tale tu na mmoja wa maaskari polisi waliompeleka ndio walioingia ofisini kwa naibu msajili.
Baada ya muda mfupi takribani dakika tano hivi, wakili wa Babu Tale na askari polisi walitoka nje kisha wakasogea pembeni wakafanya majadiliano mafupi pamoja na baadhi ya ndugu wa Babu Tale.
Comments
Post a Comment