Fahamu Madhara Ya Usukaji Wa Nywele Bandia Na Uvaaji Wa Mawigi
Katika karne ya sasa , uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususan na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana ni walimbwende zaidi.
Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.
Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni "manyoya".
Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.
Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.
1. Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio(allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.
2. Kupata mba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa(scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.
3. Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .
4. Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.
5. Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.
6. Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.
Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.
Comments
Post a Comment