Mama Wema Sepetu Asema Mtoto Wake Yupo India Kwa Matibabu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na kesi inayomkabili staa wa filamu nchini, Wema Sepetu, anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya ambapo ameshindwa kufika katika mahakama hiyo leo Mei 29, mwaka huu, kwa ajili ya kuendelea kujitetea katika kesi yake ya matumizi ya dawa za kulevya kwa madai kwamba amekwenda nchini India kufanyiwa upasuaji.
Hayo yameelezwa leo na mama mzazi wa staa huyo, Miriam Sepetu, mbele ya hakimu, Thomas Simba, baada ya Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, kuhoji kwa nini Wema hakufika mahakamani.
Wakili huyo amedai kuwa anashangaa kutomuona Wema, kwani hata ahirisho la mwisho la kesi yake hakuwepo. Baada ya kueleza hayo, Mama Wema akatoa nyaraka za Wema za kusafiria na kuieleza mahakama kuwa Wema anaumwa na amekwenda nchini India kufanyiwa upasuaji.
Wakili Kakula amesema kuwa hakuna uthibitisho wowote wa kuonyesha Wema anaumwa, hivyo akaiomba mahakama isimamie sheria. Kutokana na hoja hiyo, Hakimu Simba amesema ni kweli hakuna uthibitisho, hivyo katika tarehe ijayo uthibitisho unapaswa kuwepo, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 13, mwaka huu.
Mbali na Wema, washtakiwa wengine ni Angelina Msigwa na Matrida Abbas.Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kuzitumia.
Comments
Post a Comment